Monday, December 24, 2007

TEAK-MITIKI (tectona grandis)


Hii ni moja ya miti inayotoa mbao aghali zaidi duniani, hii ni kwa sababu mbao hii haiharibiwi kirahisi na maji kwa sababu ina mafuta yanayoteleza, pia huwa haiathiriwi na mchwa

MBEGU
Mbegu za mitiki huloekwa kwa siku 3-4 katika maji yatembeayo, au katika vyombo na kubadilishwa maji kila baada ya ya masaa 12. kabla ya kuloekwa onaziweka kwenye gunia na kufunga na kitu kizito kama jiwe ili kuzizamisha chini. Baada ya hapo unazianika mpaka zikauke vizuri




KITALU
Mbegu zipandwe kwa msitari na nafasi kati ya msitari na msitani ni sentimeta 10 na zifukiwe chini kina cha sentimeta 1. Kitalu kiwe na mwanga wa kutosha kwa sababu kwenye kivuli mbegu hazitaota na zimwagiwe maji kila siku, kilo moja ina wastani wa mbegu 1500 na uotaji ni asilimia 40-60. Mbegu zitaanza kuota baada ya wiki 4-7 na kipindi chote zinahitaji maji ya kutosha na udongo uwe hautuamishi maji.

UPANDAJI
miti hii hupandwa mara baada ya mvua ya kwanza kuanza, unaweza kutumia vipandikizi, miche au hata matawi. Kipimo ni umbali wa mita 2.5-3 kati ya mche na mche, ekari moja inatosha miche 504. miti inayongolewa kwenye kitalu inakatwa mzizi na shina na kubakia shina 25% na mzizi 75% hii husaidia kuzuia upotevu wa maji na kupata mti ulionyooka utakapoota upya.

UVUNAJI
Uvunaji wa kwanza huanza baada ya miaka 6-8 ambapo uaweza kuvuna nusu ya miti kama nguzo za kujengea, hii hufanyika ili kuipa nafasi miti inayobaki kukua zaidi.
Uvunaji wa pili ni baada ya miaka 12-15 ikifuatiwa na 20 kisha 25, katika hivi vipindi ndipo utakapopata mbao na kadri mti unavyochelewa kuvunwa ndio ukubwa na thamani ya mbao inaongezeka

LEUCAENA-VIBIRITI








Hii ni aina ya miti yenye matumizi mengi ambayo unaweza kuikuta katika miti midogo mingi pamoja kama kichaka mpaka miti mikubwa kabisa ya kutoa mbao

MATUMIZI
1-Hutumika kama chakula cha mifugo na ina protein kiasi cha 3-5% pia ina nitrogen ya kutosha kwa wanyama wenye matumbo manne (ruminants) kwa wanyama wenye tumbo moja (non ruminants) kama farasi, punda na nguruwe isitumike zaidi ya nusu ya mlo kwa sababu ina sumu inayojulikana kama mimosine ambayo inasababisha kunyonyoka manyoya

2-Pia hutumika katika kuongeza mbolea kwenye udongo kwa kiasi cha N 2-45%, P 0.2-0.4%, K1.3-4%, Ca0.8-2% na Mg 0.4-1%, hupandwa kwenye shamba linalopumzishwa au kuchanganywa na mazao ili kurutubisha ardhi.

3-Kwenye maeneo yaliyoathirika na ukataji wa miti, leucaena hutumika katika kurudisha uoto. Hii ni kwasababu inakua haraka sana na inasambaa kama moto nyikani, inaweza kupandwa kwa kumwaga mbegu na zikaachwa kuota zenyewe au kwa kupanda miche. Kama kuna sehemu unataka ijae miti haraka panda miti hii hata kama ni michache itasambaa yenyewe, ingawa kwenye sehemu zenye baridi inakua kwa tabu kidogo.

4-Mbegu zake zinaweza kuliwa baada ya kukaangwa kama bisi, hii hufanyika mara nyingi wakati wa uhaba wa chakula kwa sababu ukusanyaji wa mbugu unasumbua kidogo

5-Matumizi mengine ni mbao, kuni na fito za kujengea, miti hii hutoa mbao nyekundu ambazo zinaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali.